Tuesday, May 14, 2013

ONYO KWA WANAOUZA DAWA NA VIPODOZI KWENYE MABASI & TRENI.

 MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA
                                                            TAARIFA KWA UMMA
ONYO KWA WANAOUZA DAWA NA VIPODOZI KWENYE MABASI
Kumekuwa na tabia kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kuuza bidhaa aina ya dawa na vipodozi kwenye vyombo vya usafiri hasa treni na mabasi ya abiria. Uuzaji wa bidhaa hizi kwenye vyombo vya usafiri ni kinyume na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 ya mwaka 2003. Sheria hii inapiga marufuku kufanya biashara kwenye maeneo ambayo hayajasajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri.


Dawa na vipodozi ni bidhaa zenye sumu zinazodhibitiwa na TFDA. Bidhaa hizi zinatakiwa zihifadhiwe na kuuzwa kwenye maeneo ambayo yanakidhi matakwa ya uhifadhi na uuzaji ili kuhakikisha kuwa zinaendelea kudumisha usalama na ubora wake na hivyo kutomdhuru mtumiaji. Bidhaa hizi zikihifadhiwa mahali kwenye joto jingi, pachafu na pasipo na uangalizi wowote zinakuwa duni, kushindwa kutibu na kutengeneza sumu zinazoweza kumuathiri mtumiaji.
Maeneo yote yanayohifadhi na kuuza bidhaa hizi husajiliwa na TFDA baada ya kukidhi vigezo muhimu ikiwa ni pamoja na usafi, ukubwa wa eneo na uwezo wa kuhifadhi bidhaa husika. Kwa hali halisi, vyombo vya usafiri hususan treni na mabasi havikidhi vigezo vya kuhifadhi bidhaa za dawa na vipodozi na havitakiwi kuweka wala kutumika kuuza bidhaa hizi. Hivyo, wanaofanya biashara ya bidhaa hizi ndani za vyombo vya usafiri wanavunja sheria.

Kwa maelezo ya hapo juu, hairuhusiwi kwa mtu yeyote kufanya biashara ya kuuza dawa na vipodozi kwenye vyombo vya usafiri. TFDA inatoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na biashara hii kuacha mara moja. Wale wote watakaokamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Wananchi mnaombwa kutonunua bidhaa hizi kwenye vyombo vya usafiri kwani usalama na ubora wake ni wa mashaka na hivyo matumizi yake ni hatari kwa afya zenu.

Aidha, wananchi mnaombwa kuwafichua na kutoa taarifa TFDA pale mnapobaini wafanyabisahara wanaingia kwenye treni na mabasi kwa ajili ya kutangaza na kuuza bidhaa za dawa na vipodozi.
Taarifa itolewe kwenye kituo chochote cha Polisi au Ofisi ya afya iliyopo karibu yenu na kwenye anuani zifuatazo:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) – Makao Makuu
S. L. P 77150
Dar-es-Salaam
Tanzania
Simu: +255 22 2450751
+255 22 2450512
TFDA Kanda ya Kaskazini
S.L.P 16609, Arusha
Simu : +255 27 2547097
TFDA Kanda ya Kati
S.L.P 1253, Dodoma
Simu : +255 26 2320156
TFDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
S.L.P 6171, Mbeya
Simu : +255 25 2504425
TFDA Kanda ya Ziwa
S.L.P 543, Mwanza
Simu : +255 28 2500733
TFDA Kanda ya Mashariki
S. L. P 77150, Dar-es-Salaam
Simu: +255 22 2450751
+255 22 2450512

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...