Wednesday, May 15, 2013

WANAUME 4 WA AL- SHABAAB WAHUKUMIWA HUKO MAREKANI.

Wanaume wanne wamehukumiwa kifungo jela katika jimbo la Minnesota nchini Marekani. Wanahusishwa na kuwasajili wapiganaji kwa niaba ya kundi moja la wapiganaji wa kiisilamu nchini Somalia.
Wanne hao,Abdifatah Isse, Salah Ahmed na Ahmed Mahamud walihukumiwa jela miaka mitatu na mahakama moja baada ya kukubali mashtaka wakisema kuwa walisaidia katika kuwapa silaha kundi la al-Shabab.
Omer Mohamed alipokea kifungo cha miaka 12 kwa kushirikiana na wenzake kuwezesha mpango wao.
Viongozi wa mashtaka walipendekeza kupunguza kiwango cha miaka waliyofungwa kwa sababu wanaume hao walishirikiana na polisi katika uchunguzi.
Isse na Ahmed walikiri kusafiri Somalia mwezi Disemba mwaka 2007 na kuhudhuria mafunzo kambini. Baadaye waliondoka Somalia mwaka 2008 baada ya kupokea mafunzo.
Mahamud alisema alisaidia katika kuchangisha pesa ili wenzake waweze kusafiri kwenda Somalia.
Ingawa Mohamed hakutuhumiwa kwenda Somalia, alikiri kusaidia baadhi ya vijana waliosajiliwa kuweza kupata vyeti vya kusafiri kwenda Somalia.
Alitajwa na viongozi wa mashtaka kama kiongozi wa kijamii na mashahidi walisema kuwa alitumia elimu yake ya kidini kuwashawishi vijana kwenda vitani.
Wakili wa Mohamed alikanusha madai kuwa alihusika na kuwasajili vijana kupigana.
Al-Shabab ni kikundi cha wapiganaji wa kiisilamu nchini Somalia, na majeshi ya Kenya yakisaidiana na yale ya Muungano wa Afrika yalipambana dhidi ya wapiganaji hao na kuwafurusha kutoka Mogadishu.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...